PATA POWER BANK ZENYE UBORA WA HALI YA JUU KWA BEI NAFUU ZAIDI

PATA POWER BANK ZENYE UBORA WA HALI YA JUU KWA BEI NAFUU ZAIDI

Monday, January 19, 2015

JAJI WARIOBA ACHANGIWA NAULI ILI AKATOE SOMO LA KATIBA.



Moshi. Wananchi wa Jimbo la Vunjo mkoani Kilimanjaro wamechanga Sh200,000 za nauli ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba ili aweze kufika jimboni humo kutoa somo la Katiba.
Fedha hizo zilitolewa juzi na kukabidhiwa kwa Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia wakati akihutubia mikutano ya hadhara kwa nyakati tofauti katika miji ya Himo na Moshi Mjini kwa lengo la kuwashukuru wananchi kwa kuwaamini wagombea wa Ukawa na kuwapa ushindi katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya fedha hizo, Katibu wa Umoja wa Wanawake wa NCCR-Mageuzi, Getrude Pwila alisema kama hazitatosha kwa nauli ya Jaji Warioba, wako tayari kuchangishana kuongeza.
“Tunataka tuelimishwe hii Katiba Inayopendekezwa kwa sababu hatuko tayari kuipigia kura kwa sababu hatuielewi, hatujaiona wala kuisoma na kuielewa,” alisema Pwila kwa niaba ya wananchi wa jimbo hilo.
Katibu huyo, alimwomba Mbatia ambaye pia ni Mbunge wa Kuteuliwa, amwombe Jaji Warioba kwenda katika jimbo hilo kuendesha kongamano kama alivyofanya katika miji ya Mwanza na Dar es Salaam na wao wako tayari kumgharimia.
“Leo tunayo nusu ya nauli (Sh200,000) akikubali tuko tayari kuchangia na kujazia Sh200,000 nyingine na tunakukabidhi shati la kitenge kama alilokuwa anavaa Mandela (Nelson) ili ukamkabidhi,” alisema.
Pwila alisema wananchi wa Vunjo wanamchukulia Jaji Warioba kama Mandela wa Tanzania, ndiyo maana wamempatia shati hilo.
Jaji Warioba alipoulizwa kuhusu maombi hayo, alisema hajayapokea na hajui lolote.
Katika mkutano huo, pia wananchi walimkabidhi Mbatia suti mpya ambayo wanataka aivae atakapokwenda bungeni kuapishwa akiwa mbunge wa jimbo hilo.

Mbatia awasha moto


Kwa upande wake, Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, alimtaka Rais Jakaya Kikwete kutekeleza masuala aliyokubaliana na viongozi wa vyama vya siasa kupitia Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) mwaka jana.Mbatia alisema moja ya makubaliano hayo yalikuwa ni kufanya mabadiliko ya Katiba ya sasa ili kuruhusu kuwapo kwa tume huru ya uchaguzi ili Uchaguzi Mkuu wa Oktoba uwe wa huru na wa haki.
Vilevile, mabadiliko hayo yangeruhusu kuwapo kwa mgombea binafsi, matokeo ya uchaguzi wa rais kuhojiwa mahakamani, mshindi wa urais kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura na kuahirisha kura ya maoni hadi mwaka 2016.
Akihutubia mkutano katika Mji mdogo wa Himo, Mbatia alisema mwaka huu hawako tayari kuona Uchaguzi Mkuu unavurugwa na wasimamizi wanaopokea maelekezo ya Serikali. “Ninamwomba Rais asimamie maridhiano haya kwa masilahi mapana kwake na kwa nchi yetu kabla miezi yake hii minane aliyobakia nayo haijawa michungu kwake,” alisema.
Mbatia alisema makubaliano hayo yalikuwa ni ya utu na kwamba kwa utafiti alioufanya anaona giza mbele na hakuna uwezekano wa kupitishwa kwa Katiba Inayopendekezwa kwa vile haina maridhiano. “Naomba kama inawezekana wote tuseme Katiba Inayopendekezwa hapana, hapana, hapana! Badala ya kulumbana tuangalie kesho, hatutaki uchaguzi mkuu wa kumwaga damu,” alisisitiza Mbatia.
Mwanasiasa huyo aliyetangaza nia ya kuwania ubunge katika Jimbo la Vunjo, aliishauri Serikali iwakukutanishe haraka viongozi wa vyama vya siasa kutafuta maridhiano ya kitaifa kwa kuwa Ukawa hawako tayari kuigeuza nchi kuwa ya machafuko.

No comments:

Post a Comment