Mara nyingi wengi wetu tumekuwa katika mahusiano na wapenzi wetu lakini hali sio kama ile ya awali wakati mnaanza mapenzi yenu. Wanawake wengi wanalalamika kuwa hawaoni upendo ule waliouzoea zamani wakati mapenzi yanaanza. Hata wanaume wengine wanalalamika pia kuwa penzi limeteremka kiwango baina yao.
Mara zote hushuka huku kwa ukaribu (intimacy) hakupangiliwi au kutazamiwa bali huja taratibu pasipo wapenzi kutambua, mara lugha hubadilika, muda wakuwa pamoja hupungua, mambo huanza kufanywa kwa mazoea, vilivyo zoeleka kufanyika havionekani tena na taratibu hali hii ikikomaa huathiri hata tendo la ndoa. Katika hatua hii, wapenzi huanza kuchokana na kutotamaniana, hapa ndio kwenye upenyo wa mmoja au wote kuwaza njia mbadala. Wengi walioachana au kutalikiana nao walipitia njia hii pia.
Ili kuepuka yote haya, haunabudi kujifunza njia za kuwasha moto wa upendo kila wakati na kuongeza ukaribu (intimacy) kati yenu.
Njia za kukusaidia
1. kucheka pamoja
Kicheko ni mlango wa ukaribu, kama mwaweza kucheka pamoja basi mwaweza kulia pamoja, na hapa mwaweza kuaminiana zaidi katika kuwasiliana hisia zenu, kama waweza kuitafuta furaha katika kila kitu basi unaweza kupenya katika vyote. Usiwe mgumu na mwenye msimamo mkali katika kila kitu. Jifunze kujizuia pale unapoanza kuelekea kwenye kukasirika na badala yake tumia kucheka kama mlango wa kutokea. Kama utaanza kujizoeza hivi ukiwa nyumbani, taratibu utaweza ukiwa ofisini na hata kwingine kokote.
2. Jifunzeni kutiana moyo
Kila mmoja awe msaada na tegemeo kwa mwenzake. Jifunze kumtia moyo na kumwezesha mwenzako. Sikiliza na kufuatilia vile mwenzako afanyavyo au apendavyo. Onyesha heshima katika vitu hivyo pia. Kila upatapo nafasi mpongeze mbele za watu au hata unapokua nae peke yenu. Mjenge mwenzako mbele yawengine na kubali pongezi zote za mafanikio yenu zimwendee yeye. Mruhusu mpenzi wako ajue kuwa una mkubali katika kila afanyalo. Zaidi tunavyo wainua wapenzi wetu ndivyo wanavyotuthamini na kutunyanyua na sisi pia.
3. Jifunzeni kupenda kugusana
Nguvu ya mguso wa ukaribu kamwe haiwezi kulinganishwa na chochote. Lazima mjifunze kujenga tabia ya kugusana mara mpatapo nafasi sio tu mnapokuwa mmelala. Kugusana huku ni pamoja na kushikana mkono mkiongea au mkitembea, kukumbatia bega, kugusa au kuchezea nyewele za mwenzako na njia nyingine zozote za kuonyesha ukaribu kimwili. Wengi wetu huweza kufanya haya kidogo tunapokuwa peke yetu na kamwe sio mbele ya watu, Je, ni aibu? au nidhamu mbaya? au dhambi?
Kugusana ndio mwanzo wakuamsha hisia za kuhitajiana, (hembu jiulize kisirisiri, lini umegusana na mwenzako nje ya chumbani). Kumgusa umpendaye hukuzuia kutowaza au kutovutiwa kumgusa yeyote katika ulimwengu uliojaa wengi waliopweke wanaotamani kuguswa.
Mguso huu wa upendo haumaanishi mguso wa tendo la ndoa, ingawa pia ni vema kujifunza kuijenga lugha ya mguso wa tendo la ndoa katika mahusiano yenu.
4. Zungumzeni hisia zenu
Kati ya vikwazo vikubwa katika ustawi wa mahusiano mengi hususani ya wanandoa ni kutokuwepo kwa majadiliano. Lazima wapenzi wajifunze kuzungumza kuhusu hisia zao. Kama vile maisha yasivyo na ukamilifu, mahusiano na hata ndoa pia hazina ukamilifu. Mpenzi wako hayuko kamili na wala wewe pia sio mkamilifu. Jifunze kuzungumza na umpendaye jinsi unavyojisikia na nini kinachokusumbua. Kuendela tu na migogoro isiyosuluhishwa husababisha moyo kuwa baridi juu ya mwenzako, jiwekeeni muda kila wiki ninyi wawili kutoka ili kuzungumza mambo yenu. Mwambie umpendae yapi yanayojiri kila siku na zipi changamoto zako, mkiweza kujifunza kuwekeza katika muda wa kuwa pamoja taratibu hata muda wenu wa maongezi ya simu utaongezeka.
5. Samehe na kubali kusamehewa
Kamwe tusiache maumivu na machungu yatawale mahusiano yetu. Lazima tujifunze kuwasamehe tuwapendao na kujisamehe sisi pia. Kutofautiana katika mahusiano kupo sana, na lazima tuwape tuwapendao nafasi ya kuelezea vile vinavyowaudhi dhidi yetu. Kila hisia za mmoja wetu zinaumuhimu. Huwezi kuona vile ulivyo, mruhusu mwenzako akuambie yanayo muumiza na msameheane.
6. Linda muonekano wa mpenzi wako
Mara nyingi hatari hii hutokea tunapokuwa katika mizunguko ya huku na huko. Ukaribu na mpenzi wako hauendelezwi tu bali pia unalindwa, pia muonekano wetu lazima ume halisi na sio feki. Vile tunavyoviona katika tamthilia na filamu sio ukaribu ulio halisi. Kama tunataka tuonekane sawa na vile tunavyowaona wengine wanavyopendana basi tunakosea na kujizuia kuwa na mtazamo bora katika mahusiano yetu. Ukianza kupata ukaribu wa kweli baina yako na mwenzako utapoteza hisia ya kuhitaji ukaribu huo na mwingine yeyote, na badala yake utaanza kuulinda ukaribu mlionao.
Lengo liwe kuvitafuta vile vyote mpenzi wako alivyonavyo ambavyo hukuza ukaribu wenu. Mwenzako awe ndio mtu wa muhimu kuliko wote katika maisha yako.
No comments:
Post a Comment