PATA POWER BANK ZENYE UBORA WA HALI YA JUU KWA BEI NAFUU ZAIDI

PATA POWER BANK ZENYE UBORA WA HALI YA JUU KWA BEI NAFUU ZAIDI

Monday, January 19, 2015

CCM KUWABANA MAKADA WALIOHUSIKA NA ESCROW


Dar es Salaam. Kamati Ndogo ya Maadili ya CCM leo inaketi kutoa hatima ya makada wa chama hicho waliotajwa kuhusika katika kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow.
Kikao hicho kitakuwa chini ya Makamu Mwenyekiti wa CCM - Bara, Philip Mangula kama ilivyoagizwa na Kamati ya CCM iliyokutana wiki iliyopita.
Walioitwa katika kamati hiyo ni aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka ambaye ni mjumbe wa Halmashauri Mkuu (NEC) na Kamati Kuu ya CCM (CC) pamoja na wajumbe wa NEC, Andrew Chenge (Mbunge wa Bariadi Magharibi) na William Ngeleja (Sengerema).
Kwa kuwa uamuzi wa CC unasisitiza utekelezaji wa maazimio ya Bunge, kwa vyovyote unamlenga pia Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ambaye mpaka sasa amewekwa kiporo.
Kamati Kuu iliyofanyika Januari 13, mwaka huu Zanzibar iliazimia kuwa hatua za kimaadili zichukuliwe kwa wote waliohusika na ukiukwaji wa maadili kwenye sakata la Escrow ambao wako kwenye vikao vya uamuzi vya CCM.
Pia kikao hicho kiliitaka Serikali kuendelea kutekeleza maazimio ya Bunge kuhusu sakata hilo ambalo lilikiweka chama hicho katika wakati mgumu katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliomalizika hivi karibuni.
Kutokana na azimio hilo, Ngeleja, Profesa Tibaijuka na Chenge wanakabiliwa na adhabu ya kuvuliwa nyadhifa walizonazo ndani ya vikao vya amuzi vya CCM.
Makada hao walitajwa bungeni kuwa walipokea mamilioni ya shilingi kutoka katika akaunti ya VIP Engineering inayomilikiwa na James Rugemalira. Chenge na Profesa Tibaijuka walipokea Sh1.6 bilioni wakati Ngeleja alipokea Sh40.4 milioni.
Hata hivyo, Ngeleja anayetajwa kutaka kuwania urais anaweza kukumbwa na adhabu nyingine iwapo atabainika kuwa alikwenda kinyume na adhabu aliyopewa pamoja na wenzake watano ya kuhusishwa na ukiukwaji wa maadili kwenye mchakato wa kutaka kuteuliwa na chama hicho kugombea nafasi hiyo.
Adhabu hiyo aliyopewa Ngeleja pamoja na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, January Makamba, Bernard Membe na Stephen Wasira inamalizika Februari mwaka huu na baada ya hapo itafanyika tathimini kuona kama walizingatia masharti ya adhabu zao.
Kwa mujibu wa taarifa ya CC, ambao hawakuzingatia masharti wataongezewa adhabu.
Tayari uteuzi wa Profesa Tibaijuka umeshatenguliwa na sasa Rais Kikwete anasubiriwa kumtangaza mrithi wake na kumalizia ‘kiporo’ cha Profesa Muhongo.Maazimio ya Bunge
Azimio la pili la Bunge lilitaka Waziri wa Nishati na Madini, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Tanesco wawajibishwe, kwa kuishauri mamlaka yao ya uteuzi kutengua uteuzi wao.
Kati ya hao wote, mtu pekee ambaye mpaka sasa bado hajachukuliwa hatua yoyote ni Profesa Muhongo.
Jaji Frederick Werema ameshajiuzulu nafasi yake ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Eliakim Maswi aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini alisimamishwa kazi na Bodi ya Tanesco imeshaundwa mpya.
Bunge pia liliazimia kuwa Chenge na Ngeleja ambao walikuwa wenyeviti wa kamati za Bajeti na ile ya Katiba, Sheria na Utawala, mtawalia, kuvuliwa nyadhifa zao, jambo ambalo bado linasuasua.
Sakata la Escrow pia linaweza kuwaathiri wanasiasa hao kwa upande mwingine kwa kuwa wote bado wana nia ya kutetea nafasi zao za ubunge katika majimbo yao.

No comments:

Post a Comment