PATA POWER BANK ZENYE UBORA WA HALI YA JUU KWA BEI NAFUU ZAIDI

PATA POWER BANK ZENYE UBORA WA HALI YA JUU KWA BEI NAFUU ZAIDI

Tuesday, November 6, 2012

TATIZO LA UPATIKANAJI WA MAFUTA LITAISHA

SERIKALI imesema hali ya upatikanaji wa mafuta imeanza kurejea katika hali ya kawaida nchini na kwamba itatoa taarifa rasmi wakati wowote kabla ya kuahirishwa kwa Mkutano wa Tisa wa Bunge la Kumi Ijumaa wiki hii.



Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliyasema hayo bungeni jana baada ya kuombwa na Spika wa Bunge, Anne Makinda ambaye alikumbushwa na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema) juu ya ahadi ya Serikali ya kulizungumzia suala la uhaba wa mafuta nchini kama ilivyokuwa imeahidi Ijumaa iliyopita, kwamba taarifa rasmi ingetolewa jana, Jumatatu.



Mnyika, baada ya kipindi cha maswali na majibu bungeni alisimama na kutumia Kanuni ya Bunge namba 68 (7) kuomba mwongozo wa Spika juu ya ahadi ya Serikali kwa kuwa suala la mafuta halikuonekana katika orodha ya shughuli za Bunge kwa siku ya jana, kama Spika alivyokuwa amemwagiza Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo wa kumtaka atoe taarifa ya Serikali ifikapo Jumatatu (jana).

Akiomba mwongozo, Mnyika alisema kuwa hali ya mafuta bado sio nzuri kwani mikoani mafuta bado hayapo na kwamba suala hili halimo hata katika orodha ya shughuli za Bunge za jana.

Mnyika alisema mbali ya taarifa ya serikali kutokuwamo katika orodha ya shughuli za bunge, lakini pia kumekuwapo na kauli zinazokinzana zinazotolewa na Waziri Muhongo na Naibu waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene.

Baada ya kutoa kauli hiyo, Spika Makinda alimtaka Waziri Mkuu kutoa taarifa kwa kuwa Waziri na Naibu wake, wote hawakuwepo bungeni.



Ndipo Waziri Mkuu alisimama na kusema kauli ya Serikali itatolewa kabla ya kuahirishwa kwa shughuli za Bunge, akisema bado inashughulikiwa, huku akiongeza kuwa, hali ya upatikanaji wa mafuta imeanza kuwa nzuri.

Hata hivyo alisema hilo haliwezi kuonekana haraka kwa watu wa mikoa ya nje ya Dar es Salaam kwa kuwa kazi ya kuyasafirisha kwa malori inachukua muda.

Petroli kufichwa Pamoja na kauli hiyo ya serikali zipo taarifa zinazodai kuwa kuadimika kwa mafuta kunatokana na vitendo vinavyofanywa na wauzaji wake za kuficha kusubiri bei mpya itakayotangazwa kesho.

Mkurugenzi wa Mpango Unaoratibu Uagizaji wa Mafuta (PIC), Michael Mjinja alielezea kushangazwa na kuadimika kwa nishati hiyo na kwamba huenda wafanyabiashara wameficha bidhaa hiyo kusubiri bei mpya.

Kauli hiyo pia imeungwa mkono na mfanyabiashara maarufu nchini, Azim Dewji ambaye alidai kuwa kero ambayo Watanzania wanaendelea kupata, imetokana na wafanyabiashara wengi kushindwa kuuza bidhaa hiyo kutokana na bei ndogo iliyopo na hivyo kukosa faida.

Wakati mafuta yakiadimika katika vituo vya reja reja, Mjinja alisema kuwa kuna mafuta mengi na ya kutosha nchini na akashangaa inakuwaje baadhi ya vituo vya mafuta kukosa nishati hiyo.

Alitoa mfano kuwa kuna meli iliyomaliza kupakua mafuta juzi na kufanya kiasi kilichopo kwenye soko la ndani kuwa ni lita milioni 33 za dizeli na lita milioni 31 za petroli na kwamba kuna meli nyingine ambayo imeanza kupakua mafuta ya ndani jana.

“Takwimu hizi ni kwa mujibu wa kampuni zinazonunua mafuta nje walizotoa jana (juzi) nashangaa kuelezwa kuwa bado kuna upungufu wa mafuta,” alisema Mjinja na kufafanua kuwa jukumu lao ni kuagiza tu nishati hiyo, ila usambazaji wameachiwa Ewura.

Tatizo hilo limekuwa kubwa mikoani, lakini pia kwa jana katika baadhi ya vituo Dar es Salaam havikuwa na nishati hiyo, jambo ambalo linadaiwa kuwa ni wafanyabiashara kuyaficha kusubiri bei mpya kesho.



Ewura imeweka utaratibu wa kutangaza bei mpya kila Jumatano ya mwanzo ya kila mwezi, hali ambayo inafanya wafanyabiashra walio wengi kuficha bidhaa hiyo kusubiri bei mpya.

Dewji alisema ukosefu wa nishati hiyo kwenye vituo vingi vya mafuta umetokana na wafanyabiashara kuona bei ya sasa haiwalipi na hata wanapotaka kuzungumza na Ewura hawafanikiwi.

“Kero yote hii imetokana na jeuri ya Ewura, hawataki kukutana na wafanyabiashara kuzungumzia suala la bei,” alisema Dewji. Bei elekezi iliyotolewa na Ewura mwanzoni mwa Oktoba, petroli ilishuka kwa Sh 306 kwa lita na Sh 192 kwa lita moja ya dizeli.

Petroli kwa Dar es Salaam inauzwa Sh 1,994 kwa lita badala ya Sh 2, 300 ya Septemba, dizeli bei yake ilishuka hadi Sh 1,950 kutoka Sh 2,142. Bei ya mafuta ya taa ilibaki Sh 1,993.

Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Ewura, Titus Kaguo hakutaka kutoa ufafanuzi wowote juu ya suala hilo la mafuta, kwa maelezo kuwa masuala yote yanazungumzwa na Wizara ya Nishati na Madini.



“Hilo suala liko ngazi ya juu, muulizeni Maswi (Eliakim-Katibu Mkuu wa Wizara) ndiye mwenye uwezo wa kuzungumzia masuala hayo,” alisema Kaguo.  Maswi alisema atatoa kauli leo kuhusu suala hilo.

Hata hivyo, baadhi ya watu wanahoji, inakuwaje wafanyabiashara hao wasubiri bei mpya bila kujua kama inashuka au kupanda na kuhisi kuwapo watu ndani ya wizara husika kuvujisha ukokotoaji unaofanyika kabla ya kutangazwa.

Lakini wapo pia wanaosema huenda wafanyabiashara hao wanatumia muda mwingi kufuatilia bei ya soko la dunia na wanapoona mwelekeo ni kupanda bei ndipo nao kidogo kidogo wanaanza kuficha nishati hiyo.

No comments:

Post a Comment