POLISI imebaini
kuwa mmoja wa watuhumiwa wa mauaji ya aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Mwanza, Liberatus Barlow, alikwenda kuaga mwili wa Kamanda huyo katika uwanja
wa Nyamagana sambamba na wananchi wengine
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Lily Matola
jana alimtaja mtuhumiwa huyo kuwa ni Abdallah Petro ‘Ndayi’ (32) mkazi wa
Mjimwema mjini hapa ambaye anashikiliwa Polisi.
Kwa mujibu wa Kamanda Matola, Petro mbali na kutajwa
kuhusika na mauaji hayo, pia anadaiwa kuwa na rekodi ya kufungwa miaka 30 jela
katika gereza la Butimba kwa unyang’anyi wa kutumia silaha mwaka 2006.
Alitoka gerezani mwaka 2010 baada ya kukata rufaa
Mahakama Kuu ya Tanzania. Petro pia imebainika pia kuwa ni mdogo wa mtuhumiwa
wa kwanza katika kesi hiyo, Muganyizi Peter.
Vielelezo vyakamatwa. Kamanda Matola alisema mbali na
kuwa na uhusiano huo, Petro na mtuhumiwa mwingine, Abdurahim Ismail Athuman
‘Dula’ (28) mkazi wa Mkudi Ghana, pia mjini hapa, baada ya kukamatwa kwa
nyakati tofauti Mjimwema na Kilimahewa mwishoni mwa wiki, waliwapeleka polisi
mahali walikoficha baadhi ya mali za marehemu.
Mali wanazodaiwa kuonesha polisi ni pamoja na redio ya
mawasiliano ya Polisi na funguo za gari alilotumia kamanda Barlow siku ya tukio
la mauaji yake. Kamanda Matola alisema watuhumiwa waliwapeleka polisi katika
shimo la majitaka kwenye maeneo ya Nyanshana, jijini Mwanza walipokuwa
wameficha vitu hivyo. Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Joseph Konyo
alisema watuhumiwa baada ya kutimiza uhalifu, walitenganisha redio hiyo ya
mawasiliano ili isipatikane.
“Damu ya mtu
haipotei bure, hayo yote ni pamoja na Mungu mwenyewe, kwani sisi peke yetu
hatuwezi, wananchi mmetusaidia sana,” alisema Kamanda Konyo.
Baada ya kuonesha polisi vitu hivyo ambavyo sasa
vimechukuliwa kama vielelezo katika kesi ya mauaji ya Barlow, Kamanda Matola
alisema watuhumiwa hao walipekuliwa na kukutwa pia na kadi tatu za simu za
Vodacom na Airtel, simu ya mkononi, viatu vya ngozi na begi dogo.
Pia walikutwa na kofia mbili za kijeshi aina ya
bereti; moja ikiwa ya Polisi na nyingine ya kampuni ya binafsi ya ulinzi, sare
za kampuni ya ulinzi, mtarimbo, bisibisi, mapanga, televisheni mbili,
sub-hoofer na deki.
Alisema walipohojiwa, walidai wamekuwa wakihifadhiwa
na Ryoba Matiku ‘Mama Nyangi’ katika eneo la Nyakabungo Miembeni ambako mipango
yote ya uhalifu imekuwa ikisukwa. Mama huyo anashikiliwa pia kwa mahojiano.
Shukurani kwa wananchi
Kamanda Konyo alisema suala la ulinzi na usalama
huanzwa na wananchi kwenye familia zao na mtaa ili kujihakikishia shughuli za
kutafuta riziki halali zinafanyika kwa amani na utulivu. Mwenyekiti wa Mtaa wa
Nyanshana Mbugani, Maduhu Lutwenya aliwaomba wananchi kurudisha uhusiano wa
kutoa taarifa pale watu wasiojulikana wanapopita kwenye mitaa yao kwani
mawasiliano yangekuwapo, wahalifu hao wangekamatwa nao.
“Tuwe kitu kimoja, kwani suala la usalama si la
Mwenyekiti peke yake ni la kila mmoja, kwani Kamanda aliyeuawa hakuwa na hatia
na mtu,” alisema.
Kukamatwa kwa watuhumiwa hao kunafanya idadi ya
waliokamatwa kuhusika na kifo cha Kamanda Barlow, kuwa wanane na tayari watano
wamefikishwa mahakamani.
Kamanda Barlow aliuawa usiku kati ya saa 7 na 8 Oktoba
12, katika eneo la Kitangiri kona ya Bwiru baada ya kupigwa risasi shingoni na
kutokea kwenye taya na watu wanaodaiwa kuwa ni majambazi.
No comments:
Post a Comment