WATU wawili wamekufa katika matukio mawili tofauti,
mkoani Mara, akiwemo mwanafunzi mmoja wa shule ya msingi aliyebakwa na kisha
kunyongwa.
Inasadikiwa wauaji wake walimnyonga kwa kutumia gauni
alilolivaa na kisha kumtupa. Hayo yalisemwa na Kamanda wa polisi mkoa wa Mara,
Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa polisi, Absalom Mwakyoma, akizungumza na
waandishi wa habari mjini Musoma.
Kamanda Mwakyoma alisema mwanafunzi aliyebakwa na
kuuawa alikuwa anasoma darasa la sita katika shule ya msingi Makoko, iliyoko
katika manispaa ya Musoma na maiti yake ilitupwa eneo la Darajani manispaa ya
Musoma.
Alisema kuwa uchunguzi wa awali uliofanywa na polisi
na daktari inaonesha kuwa mwanafunzi huyo alibakwa kwanza kisha akanyongwa kwa
gauni lake alilokuwa amevaa. Kwa mujibu wa wazazi wa mwanafunzi huyo, alitoweka
nyumbani na siku mbili baadae mwili wake uliokotwa katika nyumba ambayo
haitumiki. Kamanda Mwakyoma alisema hakuna watu anayeshikiliwa kuhusiana na
tukio hilo. Kamanda Mwakyoma amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa jeshi
hilo, ili watu waliofanya unyama huo waweze kuchukuliwa hatua za kisheria
Katika tukio lingine mtu aliyejulikana kwa jina la
Kizwere Ndege (47), amekufa papo hapo baada ya kugongwa na basi la Kampuni ya
Bunda Express lenye namba za usajili T.810 eneo la Iramba, wilayani Butiama. Kamanda
Mwakyoma alisema marehemu aliyekuwa akitembea kwa miguu aligongwa na basi hilo
lililokuwa likiendeshwa na Mkazi wa Mwanza Ramadhan Karimu na kwamba chanzo cha
ajali hiyo ni mwendo kasi.
No comments:
Post a Comment