BAADA ya baadhi ya wabunge na wafanyakazi nchini, kulalamikia Sheria za
Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, hatimaye Serikali imeruhusu fao la kujitoa
kwa wanachama wa mifuko hiyo.
Serikali ilitoa tamko rasmi bungeni jana, ambapo imeridhia kuondoa
zuio la fao la kujitoa, katika kipindi hiki ambacho inajiandaa
kuwasilisha muswada wa sheria utakaokidhi matakwa ya Azimio la Bunge.
Tamko
hilo, lilitolewa bungeni jana na Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia
Kabaka, ambaye alisema Serikali imefikia uamuzi huo, baada ya kuzingatia
ushauri uliotolewa na wabunge.
Alisema fao la kujitoa kwa kawaida, linatolewa kwa masharti yanayomhusu mwanachama mmoja mmoja, katika mazingira mahususi.
Agosti,
2012 Mamlaka ya Kusimamia na Kudhibiti Mifuko ya Hifadhi ya Jamii
(SSRA), iliagiza mifuko iliyokuwa ikitoa fao la kujitoa, kusitisha
kufanya hivyo.
“Lengo kuu, lilikuwa kuwezesha mamlaka kutoa
vikokotoo vipya vya mafao vyenye manufaa kwa wanachama, bila kuathiri
afya ya mifuko husika.
“Kwa kuzingatia mchakato huu, ulioanza wa
kuangalia upya Sheria ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, Mamlaka ya
Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA),
imekwishaondoa agizo la kuzuia mifuko kutoa fao la kujitoa.
“Kufuatia
hatua hiyo, mifuko yote itaendelea kutoa fao hilo kama ilivyokuwa kabla
ya zuio hilo na kwa vigezo vile vile kwa wanachama wanaostahili kupata
fao hilo,” alisema.
Alisema hatua hiyo, itaiwezesha Serikali
kupata muda wa kutosha, kuandaa na kuleta Muswada wa Sheria unaokidhi
matakwa ya Azimio la Bunge na mahitaji ya kuwa na mfumo endelevu wa
Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.
Alisema hakuna ubishi kwamba, hoja
binafsi iliyowasilishwa na Mbunge wa Kisarawe, Suleiman Jafo (CCM) na
kuungwa mkono na wabunge ina umuhimu mkubwa.
Alisema pamoja na
mapendekezo yaliyojitokeza, Serikali iliunda kikosi kazi, ambacho
kilifanya utafiti na kuandaa mapendekezo, ili kuona iwapo kuna manufaa
ya kuendelea na mfumo uliopo au iwapo unahitajika mfumo mpya, kama
ilivyokusudiwa katika Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Hifadhi za
Jamii, kama zilivyorekebishwa katika Bunge la Aprili, mwaka huu.
Alisema
kikosi kazi kimekamilisha taarifa yake hivi karibuni na kuiwasilisha
serikalini na baada ya kuipitia taarifa hiyo, imebaini kwamba, yapo
mambo ya msingi kadhaa ambayo sharti yawe yameshughulikiwa kwanza kwa
kina kabla ya kuandaliwa kwa Muswada utakaokidhi matakwa ya hoja ya
Jafo.
Hoja hizo zilizingatia sheria iweke vifungu vinavyoruhusu
watumishi kutumia kiasi cha mafao yao ya uzeeni, kulipia mikopo ya
nyumba.
Kutoa mapendekezo ya marekebisho ya sheria, kuhakikisha
mifuko iliyoko kwenye sekta hiyo, inalinda haki za wanachama wao kwa
namna inayojitosheleza.
Akizungumza na MTANZANIA nje ya ukumbi wa
Bunge, Mbunge wa Kisarawe, Selemani Jafo alisema, amefurahishwa na
uwamuzi wa Serikali wa kuruhusu fao la kujitoa.
Hata hivyo
alisema, Serikali kuruhusu fao la kujitoa haina maana kuwa, hoja yake
imekwisha na kueleza kuwa, kilichobaki ni maandalizi ya muswada wa
sheria itakayokidhi mahitaji kulingana na Azimio la Bunge.
“Nimefurahishwa
sana uwamuzi wa Serikali wa kuruhusu fao la kujitoa, liendelee kama
ilivyokuwa zamani, hoja yangu ilikuwa na mambo mengi, lakini fao la
kujitoa ndiyo ilikuwa kilio changu kikubwa ambacho ni kilio cha
wafanyakazi.
“Kwa uwamuzi huu Serikali, mwanachama yeyote wa
mfuko wowote wa hifadhi ya jamii, hahitaji tena kusubiri hadi afikie
miaka 55, ndipo akachukue mafao yake, hii ni hatua kubwa,” alisema.
No comments:
Post a Comment