MKURUGENZI wa Mashitaka (DPP), Dk Eliezer Feleshi
ameendelea kuzuia dhamana ya Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Shekhe
Ponda Issa Ponda anayekabiliwa na mashitaka ya uchochezi na wizi wa mali zenye
thamani ya Sh milioni 59.
Kesi hiyo ilitajwa jana katika Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kwa mara ya pili kwa ajili ya washitakiwa Shekhe
Ponda na wafuasi wake 49 kupewa masharti ya dhamana.
Washitakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo saa 12:30
alfajiri wakiwa chini ya ulinzi mkali wa Polisi, wakisindikizwa na magari
manane ya Polisi, farasi, mbwa pamoja na gari la maji ya kuwasha huku askari
wengine wakiwa wamevaa mavazi rasmi ya kujikinga na silaha.
Waliingizwa kwenye chumba cha mahakama saa 2:00 asubuhi
huku nje ya kukiwa na ulinzi mkali wa askari, mbwa pamoja na kamera ya CCTV
iliyokuwa imefungwa katika ukuta wa mahakama ili kuhakikisha hakuna mtu
anayeingia na silaha.
Kila mtu aliyeingia katika eneo la mahakama alihojiwa
na kukaguliwa na Polisi ambapo wafuasi wengi wa Shekhe Ponda waliofika
kusikiliza kesi hiyo walizuiwa kuingia katika eneo hilo kwa kuhofia
wangesababisha vurugu.
Wakili wa Serikali, Tumaini Kweka alidai upelelezi wa
kesi hiyo umekamilika na kumuomba Hakimu Victoria Nongwa anayesikiliza kesi
hiyo kutoa uamuzi wa maombi ya dhamana kwa washitakiwa.
Hakimu Nongwa alisema dhamana ipo wazi kwa mshitakiwa
wa pili hadi wa 50 endapo watatimiza masharti ya kuwa na mdhamini anayefanya
kazi katika taasisi inayofahamika, atakayesaini hati ya Sh milioni moja.
Hata hivyo, alisema Shekhe Ponda ataendelea kubaki
rumande kwa kuwa Mkurugenzi wa Mashitaka aliwasilisha mahakamani hapo hati ya
kuzuia asipewe dhamana, hivyo hawawezi kutoa dhamana hadi DPP atakapowasilisha
hati ya kuiondoa hati ya kuzuia dhamana.
DPP aliwasilisha hati hiyo chini ya kifungu cha 84 (4)
cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002, inayompa mamlaka DPP
kufunga dhamana kwa mshitakiwa anayekabiliwa na makosa yanayodhaminika.
Kwa kifungu hicho, Mahakama inafungwa mikono na hivyo
haina mamlaka ya kuipinga hati hiyo hadi DPP atakapoiondoa hati hiyo mahakamani.Katika
hati hiyo, DPP ametaja sababu mbili za kuzuia dhamana hiyo; ya kwanza kwa ajili
ya usalama na sababu ya pili ni maslahi ya Jamhuri.
Katika kesi hiyo, washitakiwa hao akiwamo Zaida Yusuf
mwenye umri wa miaka 100, wanatetewa na Wakili wa Kujitegemea, Nassor Mansoor.
Wote wanakabiliwa na mashitaka matano ambapo Oktoba 12
mwaka huu, katika eneo la Chang’ombe Markasi wanadaiwa kula njama na kuingia
kwa nguvu katika kiwanja kinachomilikiwa Kampuni ya Agri Tanzania Ltd kwa nia
ya kujimilikisha kiwanja hicho isivyo halali.
Aidha, inadaiwa kati ya Oktoba 12 na 16, mwaka huu,
Chang’ombe Markaz pasipo uhalali, washitakiwa wote katika hali iliyokuwa
ikichangia uvunjifu wa amani, walijimilikisha kwa nguvu ardhi ya kampuni hiyo.
Pia wanadaiwa waliiba vifaa na malighafi, matofali
1,500, nondo na tani 36 za kokoto mali zote zina thamani ya Sh milioni 59.7.
Katika mashitaka ya uchochezi yanayomkabili Shekhe Ponda peke yake, inadaiwa
katika eneo hilo la Chang’ombe Markaz akijiita Katibu wa Jumuiya na Taasisi za
Kiislamu, aliwashawishi wafuasi wake ambao ni washitakiwa hao kutenda makosa
hayo
Kesi imeahirishwa hadi Novemba 15, mwaka huu
watakaposomewa maelezo ya awali.
Wakati huo huo, kundi la wafuasi wa Shekhe Ponda
waliozuiwa kuingia mahakamani, walisikika wakilalamika kuwa Waislamu duniani
kote wanakandamizwa na hata hapa nchini pia na kushauriana waondoke kwa kuwa
mahakama ni ya dini ya Kikristo, waliyodai inathaminiwa.
No comments:
Post a Comment