PATA POWER BANK ZENYE UBORA WA HALI YA JUU KWA BEI NAFUU ZAIDI

PATA POWER BANK ZENYE UBORA WA HALI YA JUU KWA BEI NAFUU ZAIDI

Thursday, September 11, 2014

'Bunge la katiba litaendelea kama ilivyopangwa'.Sitta

Dodoma. Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta ‘amekomaa’ kuhakikisha Bunge Maalumu la Katiba linafanya kazi kwa kasi na kukamilisha kila kitu ifikapo tarehe yake ya mwisho, Oktoba 4, ikiwamo kupiga kura za kupitisha Katiba inayopendekezwa kazi ambayo amesema itafanywa hadi nje ya nchi kwa wajumbe watakaokuwa huko.
Sitta alilazimika kutoa matamko mawili kwa nyakati tofauti, mara ya kwanza wakati kikao cha Bunge kilipoanza jana akieleza jinsi Rasimu ya Katiba inayopendekezwa itakavyokamilika ifikapo Septemba 21 na baadaye mchana wakati akiahirisha Bunge alipotangaza mikakati ya kukusanya kura za wajumbe hadi nje ya nchi kuanzia Septemba 26, mwaka huu.
Sitta alitumia fursa hiyo kuwataka wajumbe wa Bunge hilo watakaokuwa nje ya nchi kwa matibabu au sababu nyingine kuacha mawasiliano yao ili waweze kupiga kura wakiwa hukohuko.
Alisema uongozi wa Bunge umeanza kufanya mawasiliano na balozi mbalimbali za Tanzania nje ya nchi ili wawepo watumishi wake watakaokula kiapo cha kisheria ili wasimamie upigaji kura.
Kauli za Sitta zimekuja siku moja baada ya Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) kuweka bayana makubaliano baina ya wajumbe wake na Rais Jakaya Kikwete kuwa hataongeza muda wa uhai wa Bunge hilo, hivyo litakoma Oktoba 4, mwaka huu na hakutakuwa na upigaji wa kura ya maoni kupitisha Katiba hiyo hadi baada ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 2015.
Kauli za Sitta
Akizungumza bungeni kwa kujiamini lakini bila kugusia ratiba ya Bunge hilo iliyokuwa inafikia Oktoba 30, mwaka huu, Sitta alisema ratiba ya Bunge hilo itaendelea kama tangazo la Rais katika Gazeti la Serikali linavyosema.
GN hiyo namba 254 iliyotolewa Agosti Mosi, mwaka huu, ililiongezea Bunge hilo siku 60 ambazo zinamalizika Oktoba 4, mwaka huu baada ya siku 70 za awali kumalizika bila kupatikana katiba inayopendekezwa.
“Kwa taarifa tu na msisitizo, ni kwamba ratiba yetu ya Bunge Maalumu inaendelea kama ilivyopangwa,” alisema Sitta huku akishangilia kwa makofi na wajumbe waliokuwamo.
“Siku 60 za Bunge hili ambazo ni nyongeza ya siku tulizopewa na Rais kwa mujibu wa sheria usipohesabu siku za Jumamosi, Jumapili na sikukuu, zinaishia tarehe 4 Oktoba,” alisema Sitta.
Alisema kikao cha Kamati ya Uongozi kilichoketi juzi, kimeelezwa kuwa Bunge hilo linakwenda vizuri na kwamba Kamati ya Uandishi imejipanga kuwapatia Rasimu ya Katiba Septemba 21, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment