SERIKALI imeagiza Mamlaka ya Udhibiti wa
Nishati na Maji (Ewura), kuchukua hatua za kisheria dhidi ya kampuni zote
zitakazokaidi kuuza mafuta kwa sasa, hali iliyosababisha usumbufu mkubwa kwa
wananchi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini,
Eliakim Maswi alitoa tamko hilo jana Dar es Salaam baada ya kupokea taarifa ya
Ewura na Kampuni inayoratibu uagizaji wa mafuta wa pamoja (PIC) iliyoonesha
kuwa kuna akiba ya mafuta inayotosha kutumika kati ya siku 10 na 14.
“Hatuwezi kuona wananchi wanateseka wakati
kuna mafuta ya kutosha nchini, wale ambao hawataki kuuza chukueni hatua
haraka,” alisema Maswi.
Awali, Mkurugenzi wa Petroli wa Ewura, Godwin
Samwel alipoulizwa sababu za kukosekana kwa nishati hiyo, ambako ilielezwa kuwa
jana baadhi ya mikoa haikuwa na nishati hiyo kabisa, alijitetea kuwa ni kweli
mafuta yapo.
Samwel alifafanua kuwa uhaba huo umetokana na
kampuni kubwa kuamua kuuza mafuta hayo kwa vituo vya kampuni zao na kuvikatalia
vituo ambavyo havina kampuni kubwa kununua mafuta hayo, hali ambayo imezua
kizaazaa cha mafuta nchini huku mikoani hali ikiwa mbaya zaidi.
“Ndio maana utakuta vituo vingine vina mafuta
na vingine havina,” alisema Samwel na kutaja sababu nyingine ya upungufu huo
kuwa ni kuwepo meli zinazopakua mafuta ya kwenda nje ya nchi na migodini kwa
muda mrefu katika boya la KOJ wakati meli zenye mafuta ya ndani
zikisubiri.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya PIC, Shaniff
Mansour alisema hadi juzi jioni kiasi cha mafuta kilichopo nchini kilikuwa
dizeli lita milioni 34.1, petroli lita milioni 20.6, jet 1 lita milioni 15.6 na
mafuta ya taa lita milioni 5.2.
Mansour alisema kiasi hicho cha mafuta
kinatosha kutumika ndani ya siku 10 na akaongeza kuwa kuanzia jana meli
nyingine yenye mzigo wa mafuta imeanza kupakua mafuta katika boya la KOJ ambako
dizeli ni tani 23, 700 na petroli ni tani 14, 800 hali inayozidi kuongeza
upatikanaji wa bidhaa hiyo.
Mansour pia alisema mafuta ambayo yako nchini
yakisubiri kusafirishwa nje (Transit) ya nchi ni mengi zaidi kuliko mafuta ya
ndani na akataja kuwa mafuta ya nje; dizeli ni lita milioni 46.6, petroli lita
milioni 31.3 na jet 1 ni milioni 4.9 na mafuta ya taa ni lita milioni
1.2.
Kutokana na hali hiyo, mbali na kuwabana
wanaosusa kuuza mafuta, Maswi aliagiza Serikali ichukue nusu ya mafuta
yanayosafirishwa nje ya nchi ili yatumike hapa nchini.
“Naagiza kampuni ziuze mafuta mikoani na hata
vituo ambavyo havina kampuni mama viuziwe mafuta kupunguza tatizo hili,”
alisema Maswi na kuitaka Ewura kuhakikisha magari ya mikoani yanapakia mafuta
kwenye maghala yalikohifadhiwa mafuta.
Aliisisitizia Ewura kuwa kampuni ambayo
haitaki kuuza mafuta ichukuliwe hatua haraka.
Alitaka pia agizo la kuuza mafuta yaliyokuwa
yanasafirishwa nje lianze kutekelezwa haraka na akashangaa kuwa haijawahi
kutokea mafuta yanayosafirishwa nje yawe mengi kuliko yanayotumika ndani ya
nchi.
No comments:
Post a Comment