Dar es Salaam. Wafanyabiashara waliokuwa wakifanya biashara katikati ya jiji na kuondolewa kutokana na ujio wa Rais wa Marekani, Barack Obama, wamelalamika kuwa sasa wanakabiliwa na maisha magumu.
Obama anatarajia kuwasili nchini kesho katika ziara ya kikazi ya siku mbili huku akiambatana na ujumbe wa watu wapatao 700.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wafanyabishara hao walisema kuondolewa huko kumewafanya kukosa kipato walichokuwa wakikipata hivyo kusababisha ugumu wa maisha.
Frank Mkama alilalamika: “Hapa Serikali isiseme kuwa wanafanya usafi wa jiji kwa kuwaondoa wafanyabiashara hii si kweli! Mbona hawakufanya zamani, hapa ni Obama ndiyo amesababisha sisi tukaondolewa.”
“Hivi sasa maisha yangu yamekuwa magumu. Kipato ambacho nilikuwa nakipata hapa na kula na familia yangu sasa sikipati.”
Naye, Elizabeth Makata alilalamika Serikali ilipaswa kuwaandaa wananchi kwa kuwaeleza ujio huo wa Obama watanufaika vipi na si kuwafanya waathirike kwa kuvunjiwa maeneo yao.
Alielezea wasiwasi kuwa huenda baada ya ziara hiyo wakashindwa kuendelea na biashara kwa kuwa watakuwa wamekula mitaji.
Kwa upande wake, Ramadhan Issa alisema ziara hiyo ya Rais Obama imeathri maisha yake kutokana na kuvunjiwa kibanda alichokuwa akifanyia biashara hivyo hajui hatima ya maisha yake.
Kadhalika askari polisi wakionekana kuongezeka katikati ya jiji wakipita huko na kule kuhakikisha hali ya usalama inaimarika.
Pia hali ya usafi imeendelea kuimarika kutokana na ujio kutokana na juhudi zinazoendelea kufanywa kwa lengo la kusafisha mazingira.
Licha kwamba wafanyabiashara hao wameondolewa hivi karibuni baadhi yao wameanza kurejea kuendelea na shughuli zao kama kawaida.
No comments:
Post a Comment