SERIKALI imeamua kutoa zawadi ya gari na fedha kwa mtu yeyote atakayeongoza kudai risiti za bidhaa au huduma atakayopatiwa.
Uamuzi huo wa serikali umelenga kuwabana wafanyabiashara na watoa huduma wanaokwepa kulipa kodi za serikali.
Akitangaza uamuzi huo jana bungeni, Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Saada Mkuya, alisema wananchi watapaswa kuwataja wafanyabiashara watakaokataa kuwapa risiti hizo baada ya kuwauzia bidhaa.
Mkuya pia alitangaza namba za simu ambazo wananchi watapiga bure na kuwaomba wabunge wasaidie kuwaarifu wananchi kuhusu namba hizo ambazo ni 0800110016 kwa watumiaji wa Voda na TTCL, Airtel 0786800000 na Tigo 0713800333.
Alisema kuwa namba hizo watazibandika maeneo mbalimbali na kuzitangaza kwenye vyombo vya habari na kila mwananchi atakayechukua risiti ya malipo ya bidhaa au huduma ataingizwa kwenye utaratibu wa kupata zawadi.
Mkuya alifafanua kuwa utaratibu wa kutoa zawadi kwa washindi utafanyika kila wiki, mwezi na baadaye kwa mwaka ambapo zawadi hizo ni pamoja na gari na fedha taslimu.
Utaratibu huu utaanza Julai mosi, hivyo akawataka wananchi kuhamasika kudai risiti kila wanaponunua bidhaa, vile ile wafanyabiashara kujenga utamaduni wa kutoa risiti hizo.
Kuhusu mashirika kuorodheshwa kwenye Soko la Mitaji na Hisa la Dar es Salaam (DSC), alisema kuwa lazima liwe na vigezo kama vile historia nzuri ya utendaji na kutengeneza faida kwa miaka isiyopungua mitatu kwa sababu lengo lao ni kuongeza mtaji.
Aliongeza kuwa shirika au kampuni inapaswa kufanya maombi ya hiari ndipo isajiliwe baada ya kutimiza masharti hayo.
Alizitaja baadhi ya kampuni na taasisi zilizomo DSE kuwa ni Benki ya NMB, TOL, TCC, CRDB, TBL, Swissport, Twiga na Tanga Cement.
Aliyataja mashirika mengine ambayo yako kwenye mchakato wa kuingia hivi karibuni kuwa ni Mtibwa Sukari, Kilombero Sukari, Mbeya Sementi, Tanalec, Alaf, NBC na Airtel.
No comments:
Post a Comment