PATA POWER BANK ZENYE UBORA WA HALI YA JUU KWA BEI NAFUU ZAIDI

PATA POWER BANK ZENYE UBORA WA HALI YA JUU KWA BEI NAFUU ZAIDI

Tuesday, August 5, 2014

Mjumbe wa UKAWA atinga bungeni

Wakati wajumbe wa Bunge la Katiba wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wakiendelea na msimamo wa kususia vikao vinavyotarajiwa kuanza leo mjini Dodoma, mmoja wa wajumbe wake jana aliripoti bungeni na kujiandikisha. 
Mjumbe huyo, Clara Mwatuka ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu (CUF), alionekana katika Viwanja vya Bunge saa 6:30 mchana akiwa ameongozana na wabunge kadhaa wa CCM wakiwamo Livingstone Lusinde (Mtera) na Jerome Bwanausi (Lulindi).
CUF ni moja ya vyama vinavyounda Ukawa, pamoja na Chadema na NCCR Mageuzi na tayari viongozi wakuu wa vyama hivyo, Profesa Ibrahim Lipumba, Freeman Mbowe na James Mbatia wametangaza kwamba wajumbe wote wanaotokana na umoja wao hawatashiriki vikao vya Bunge hilo.
 
Mwatuka baada ya kujaza fomu maalumu za kujiandikisha, alielekea lango la Magharibi na kuingia kwenye gari la Bwanausi.
Awali, alipoulizwa kwenye Viwanja vya Bunge kuhusu kuwapo kwake Dodoma, alikataa kuzungumza lakini alikiri kujiandikisha bungeni.
 
Baadaye alipoulizwa imekuwaje akajiandikisha ilhali uongozi wa chama chake umesema hawatashiriki, Mwatuka alijibu: “Kwa hapo ni mapema sana kuzungumzia suala hilo, nitazungumza kesho (leo) kule bungeni ukinitafuta.”
 
Hata hivyo, baada ya dakika kama 30 kupita, Mwatuka alimpigia simu mwandishi na kumwambia: “Sasa kuhusu mimi kuja Dodoma, ni kweli kwamba niko hapa maana nasomesha na nilipofika nimeamua kwenda pale bungeni kuripoti.”
 
Aliogeza: “Ila mimi pamoja na kujiandikisha, sitashiriki vikao vya Bunge mpaka hapo tutakapokuwa tumepewa mwongozo, maana tuliambiwa kwamba majadiliano yanaendelea kwa hiyo tukiruhusiwa nitakwenda, vinginevyo sitashiriki kabisa, ndiyo hivyo.”
 
Bwanausi kwa upande wake alisema alimpa lifti Mwatuka kutoka Dar es Salaam baada ya mbunge huyo wa CUF kuomba msaada wa usafiri kwenda Dodoma.
 
“Ni jambo la kawaida, tulionana Dar es Salaam na akaniuliza iwapo ninakwenda Dodoma na mimi kweli nafasi ilikuwapo kwenye gari, kwa hiyo tumekuja naye hadi hapa, sasa zaidi ya hapo mimi sifahamu,” alisema.
 
Wajumbe kutoka Zanzibar na wale wa kundi la 201 ndiyo waliokuwa wengi katika usajili wa jana na wajumbe ambao wanatokana na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hasa kutoka Tanzania Bara wakionekana wachache.
 
Milango yote ya kuingia katika eneo la Bunge ilikuwa imefungwa na kuacha lango moja tu la Magharibi, hali iliyosababisha baadhi ya wajumbe kuhangaika hadi pale walipopata msaada wa polisi waliokuwa wakilinda
Mkutano wa Bunge Maalumu ambao unafanyika kwa mara ya pili, unatarajia kuchukua miezi miwili ambayo wajumbe wake wanapaswa kuitumia kukamilisha kazi ya kupitia sura 15 za Rasimu ya Katiba zilizosalia na kupiga kura kuamua kuhusu sura mbili zinazohusu Muungano.
 
Katika mkutano uliomalizika Aprili mwaka huu, wabunge walikuwa wametumia zaidi ya siku 70 na walifanikiwa kupitia sura ya kwanza na sita ambazo hata hivyo, hazikupigiwa kura.
 
Hadi jana jioni Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta alikuwa akiongoza kikao cha Kamati ya Uongozi, lakini hakukuwa na taarifa rasmi kuhusu ratiba wala ajenda za mkutano unaotarajiwa kuanza leo.
 
Wabunge wapata ajali
Katika tukio jingine, Mbunge wa Tabora Mjini, Ismail Aden Rage na Mbunge wa Viti Maalumu, Munde Tambwe wamenusurika kifo baada ya gari walilokuwa wakisafiria wakati wakitokea Tabora kwenda Dodoma kupata ajali.
 
Wabunge hao wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma na hali zao zilikuwa zinaendelea vizuri.
 
Akizungumza akiwa katika Wodi Namba 18, Rage alisema amepata majeraha katika bega la kushoto na eneo la nyuma ya mgongo baada ya dereva wa gari walilokuwa wakisafiria kujaribu kulipita lori lililokuwa mbele yao, lakini ghafla lori hilo likaingia katikati ya barabara.
 
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Ezekiel Mpuya aliwataja majeruhi wengine wa ajali hiyo iliyotokea katika eneo la Chigongwe, Dodoma kuwa ni Issa Chimwaga (31), Mwanahamisi Ramadhani (34) na dereva John Hoya (32) ambaye hakuuumia.
 
Alisema vipimo vimeonyesha kuwa mbali na kupata majeraha usoni na kichwani, Munde pia amevunjika mkono wakati Rage ameteguka bega la kushoto

Monday, August 4, 2014

"Siwezi kujadili upuuzi huu" asema Rais Kikwete kuhusu tetesi kuwa alimuokoa Ridhiwani baada ya kukamatwa na dawa za kulevya!





TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Sina muda kujadili upuuzi huu kuhusu Ridhiwani – Rais Jakaya Kikwete

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa ni mkusanyiko wa upuuzi mtupu madai kuwa yeye Rais alishiriki kumwokoa mtoto wake, ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Chalinze Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete ambaye alikuwa amekamatwa na madawa ya kulevya nje ya nchi.
 
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa Urais ni taasisi kubwa sana nchini na hivyo yeye akiwa Rais hawezi kujiingiza katika ubishani na watu wa mtaani, kama ambavyo wanataka baadhi ya watu wanamsukuma ili ashiriki katika maneno hayo ya mitaani.
 
“This is nonsense – ni mkusanyiko wa upuuzi. Sina muda wala siwezi kupoteza nguvu yangu kujadili upuuzi na ujinga wa namna hiyo,” amesema Rais Kikwete usiku wa Jumamosi, Agosti 2, 2014, wakati alipozungumza na Watanzania wanaoishi katika Marekani kwenye Hoteli ya Marriot Washington, mjini Washington D.C.
 
Rais Kikwete ambaye yuko katika ziara ya kikazi ya siku tisa  Marekani alitoa majibu hayo baada ya kuwa ameulizwa kuhusu madai yaliyotolewa Julai Mosi, mwaka juzi, 2012 na Katibu Mkuu wa Chama cha CHADEMA, Wilbroad Slaa, madai hayo yamempeleka mahakamani.
 
Amesema Rais Kikwete: “Hatuwezi sisi kujiingiza katika shughuli ya kupoteza muda kwa kushiriki upuuzi na ujinga. Haya ni maneno ya kipuuzi yanayosemwa na watu ambao kazi yao usiku na mchana ni kuota jinsi ya kuyumbisha ajenda yetu ambayo imefanikiwa sana katika kubadilisha hali ya maisha ya Watanzania.’
 
Amesisitiza Rais Kikwete: “Urais ni taasisi kubwa sana. Rais wa nchi yetu hawezi kujiingiza katika ubishani na watu wa mitaani. Kwanza huyo Ridhiwani amemfikisha Slaa kortini na mpaka leo hata kesi yenyewe haijatajwa.”
 
Kuhusu swali jingine aliloulizwa kuhusu suala hilo, kuwa Rais Kikwete alitia saini mikataba 12 na uongozi wa Jamhuri ya Watu wa China kama sehemu ya masharti ya kuachiwa kwa Ridhiwani, Rais Kikwete amesema:
 
“Naipenda nchi yangu kiasi cha kwamba siwezi kufikiria hata kuiweka rehani. Haya ni maneno ya kipuuzi tu, yenye kutafuta kututoa kwenye ajenda zetu nzuri. Hatuna muda nayo, sisi tunaelekeza nguvu zetu kwenye mambo ya maana ya kuleta mabadikio katika ustawi wa Watanzania.”


Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam

ANGALIA PICHA ZA MBUNGE RAGE APATA AJALI AKIWA NJIANI KUELEKEA DODOMA

Mbunge wa Tabora Mjini (CCM) Ismail Aden Rage, ambaye pia ni mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, akiwa amelazwa kwenye hospitali ya Rufaa, Dodoma, Jumatatu Agosti 4, 2014. Rage alipata ajali eneo la Chigongwe, nje kidogo ya Manispaa ya Dodoma, wakati akielekea mjini humo tayari kushiriki vikao vya Bunge Maalum vinavyoanza Jumanne Agosti 5, 2014 

Mbunge wa Sikonge mkoani Tabora kupitia CCM, ambaye pia ni Mujumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Said Nkumba, akimjulia hali Rage, hospitalini mjini Dodoma, Jumatatu Agosti 4, 2014.