PATA POWER BANK ZENYE UBORA WA HALI YA JUU KWA BEI NAFUU ZAIDI

PATA POWER BANK ZENYE UBORA WA HALI YA JUU KWA BEI NAFUU ZAIDI

Sunday, June 23, 2013

FAIDA ZA KIAFYA ZA KITUNGUU SWAUMU. (Garlic)


FAIDA ZA KIAFYA ZA KITUNGUU SWAUMU(GARLIC)


Kitunguu swaumu ni jamii ya vitunguu ambayo kwa kitaalamu huitwa Allium sativum. Jamii hii ilianza kutumika katika mabara mbalimbali duniani hususani Asia, Afrika na Ulaya takribani miaka 6000 iliyopita. Matumizi makuu nyakati hizo yakiwa viungo katika mboga na tiba.

Kitunguu swaumu kimetajwa kwenye vitabu mbalimbali vya dini vikielezea faida zake katika kutibu maradhi mbalimbali yasababishwayo na bakteria, matatizo katika mapafu, matatizo katika mfumo wa umen'genyaji chakula, na matatizo ya kuishiwa nguvu.

Historia inaonesha kuwa, vitunguu swaumu vilianza kutumika China mwaka 510 K.K na pia vilitumiwa na wanajeshi wa Ugiriki na Roma. Aidha wasafiri wa vyombo vya baharini na vijijini pamoja na wakulima barani Afrika walivitumia sana.

  
Mwaka 1858, mtafiti na mwanasayansi wa nyakati hizo, Louis Pasteur aligundua uwezo wa kitunguu swaumu katika kuua vimelea mbalimbali vinavyosababisha magonjwa, na hivyo vikaanza kutumika kama dawa ya kusafishia vidonda na kuzuia kidonda ndugu hasa zama za vita ya kwanza na pili ya dunia. Isitoshe, mpaka sasa zipo dawa kadhaa zilizotengenewa kwa kutumia jamii hii ya vitunguu swaumu ikiwemo dawa ya kusafisha mdomo (mouth wash) ingawa watumaiji wake wengi huilalamikia dawa hiyo kwa sababu ya harufu mbaya ya dawa hiyo inayowasababishia kunuka kwa mdomo.

Faida za vitunguu swaumu

Katika tafiti mbalimbali vitunguu swaumu vimeonekana kuwa na uwezo wa kutibu maambukizi ya bakteria, fangasi na virusi vya aina mbalimbali. Aidha husaidia kuzuia magonjwa ya moyo ikiwemo kuondoa lijamu katika mishipa ya damu na hivyo kusaidia katika kurekebisha shinikizo la damu. Faida nyingine za vitunguu swaumu ni pamoja na
  • Kutibu saratani ikiwemo saratani ya tumbo na utumbo mkubwa. Tafiti zinaonesha idadi ndogo ya wagonjwa wa saratani katika nchi ambazo wakazi wake wana utamaduni wa kutumia vitunguu swaumu kwa wingi.
  • Vitunguu swaumu husaidia kudhibiti kiwango cha sukari katika damu. Hata hivyo inashauriwa kwamba wagonjwa wa kisukari wanaotumia sindano za insulin wasitumie kitunguu swaumu kwa wingi mpaka watakaposhauriwa na daktari.
  • Huzuia kusanyiko la chembe sahani zinazosaidia kuganda kwa damu (platelet aggregation)
  • Husaidia ufyozwaji wa thiamin, hivyo kusaidia kuepusha mwili na ugonjwa wa beriberi
  • Ina kiasi kikubwa cha vitamini C ambayo husaidia kuzuia ugonjwa wa kiseyeye
  • Hutumika kutibu magonjwa nyemelezi kama toxoplasmosis, hasa kwa watu wenye upungufu wa kinga mwilini.
Ushahidi wa Kitafiti

Katika utafiti uliofanyika nchini Czech ilionekana kuwa matumizi ya vitunguu swaumu yalisaidia sana katika kupunguza kusanyiko la lijamu (cholesterol) pamoja na mafuta yasiyofaa mwilini (low density lipoproteins) katika mishipa ya damu. Aidha, mwaka 2007 BBC iliripoti matumizi ya vitunguu swaumu katika kusaidia kumkinga mtumiaji dhidi ya aina fulani ya mafua iliyosababishwa na virusi. Mwaka 2010, ulifanyika utafiti mwingine ambao ulijumuisha wagonjwa 50 wenye shinikizo la damu sugu ambalo lilikuwa ni vigumu kudhibitiwa hata kwa matibabu yaliyozoeleka ya dawa na njia nyingine. Kama njia ya kuchunguza ufanisi wa vitunguu swaumu katika kutibu shinikizo la damu, baadhi ya wagonjwa hao walipewa vitunguu swaumu wakati wengine walipewa dawa isiyohusika na matibabu ya shinikizo la damu (au placebo). Ilionekana kuwa wale waliopewa vitunguu swaumu kama dawa ya shinikizo la damu walionesha maendeleo mazuri kwa vitunguu swaumu kuweza kushusha vizuri kiwango cha shinikizo la damu, hususani systolic pressure, tofauti na wale waliopewa placebo.

Nini siri ya kitunguu swaumu?

Sifa kuu zinazokifanya kitunguu swaumu kuwa na uwezo na faida zilizoainishwa hapo juu ni kule kuwa kwake na viasili kadhaa (ingredients) ambavyo vinafanya kazi tofauti tofauti. Uwezo wake wa kiutendaji unatokana na mambo yafuatayo;
  • Vina uwezo wa kusababisha kutanuka kwa mishipa ya damu (vasodilation) kwa kubadilisha polysulfides zilizopo ndani yake kuwa hydrogen sulfides kwenye seli nyekundu za damu.
  • Husaidia uthibiti wa kiwango cha sukari mwilini kwa kushusha kiwango cha kemikali ya homocystine na kupunguza madhara ya kisukari.
  • Iwapo vitapondwa pondwa vizuri, vitunguu swaumu hutoa kemikali iitwayo Allicin ambayo ni dawa dhidi ya bateria, na phytoncide ambayo huua fangasi wa aina mbalimbali.
  • Harufu mbaya ya kitunguuu swaumu hutokana na gesi aina ya hydrogen sulfide ambayo inayotolewa baada ya kuvila.
Nini Madhara ya vitunguu swaumu?

Ukiacha faida zake, vitunguu swaumu pia vina hasara na madhara mbalimbali kwa mtumiaji. Madhara hayo ni pamoja na;
  • Harufu mbaya mdomoni ambayo hutokana na kemikali ya AMS (allyl methyl sulfide). Harufu mbaya hii, hata hivyo, yaweza kupunguzwa kwa kunywa maziwa au kunywa maji mengi.
  • Kwa baadhi ya watumiaji, vinaweza kuwaletea mzio au mcharuko mwili (allergies au inflammatory reactions)
  • Kichefuchefu, Kutapika na kuharisha.
  • Huweza kusababisha hatari ya kuvuja damu, kwa sababu huzuia kazi ya seli sahani (platelets) zenye kusaidia kuganda kwa damu kushindwa kufanya kazi yake vizuri, na hususani kwa mama wajawazito, baada ya upasuaji au mara baada ya kujifungua.
  • Huingiliana katika utendaji kazi wake na dawa kadhaa kama vile warfarin, antiplatelets, saquinavir, dawa za shinikizo la damu kwa ujumla hasa calcium channel blockers, na antibiotiki za jamii ya quinolone kama vile ciproflaxacillin.
  • Aidha, vinaelezwa pia kuwa na madhara kwa wanyama jamii ya paka na mbwa.

No comments:

Post a Comment