PATA POWER BANK ZENYE UBORA WA HALI YA JUU KWA BEI NAFUU ZAIDI

PATA POWER BANK ZENYE UBORA WA HALI YA JUU KWA BEI NAFUU ZAIDI

Tuesday, November 6, 2012

BANDARI YAONGOZA KWA RUSHWA YA UNUNUZI VIFAA

MAMLAKA ya Bandari Tanzania (TPA), imetajwa kuongoza kwaviashiria vya rushwa katika ununuzi wa bidhaa na huduma unaosimamiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA).



Mkurugenzi Mtendaji wa PPRA, Ramadhani Mlinga alisema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ukaguzi wa ununuzi katika taasisi za umma uliofanyika hadi Juni 30.

Mlinga alisema walipotumia kanuni za kupima rushwa katika ununuzi, TPA ilibainika kuongoza miongoni mwa taasisi za umma zilizokutwa na viwango vya juu vya uwezekano wa kuwapo rushwa kwa zaidi ya asilimia 20 ya shughuli za ununuzi.

Mbali na TPA iliyokuwa na asilimia 44 ya viashiria vya rushwa, ilifuatiwa kwa karibu na Wizara ya Mambo ya Ndani katika mradi wa ujenzi wa makao makuu ya kikosi cha Zimamoto iliyokuwa na asilimia 41 ya viashiria vya rushwa.



Taasisi ya tatu kwa kuwa na viashiria vingi vya rushwa kwa mujibu wa PPRA, ni Wizara ya Maji na Umwagiliaji katika mradi wa maji Chalinze iliyokuwa na asilimia 40.

Nyingine ni Halmashauri ya Wilaya ya Kyela (28%), Halmashauri ya Wilaya ya Makete (27%), Halmashauri ya Jiji la Mbeya (28%), Halmashauri ya Wilaya ya Tabora (20%), Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe (28%), Chuo cha Usafirishaji cha Taifa (27%) na Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga (23%) Kuhusu ukaguzi wa miradi kwa thamani ya fedha, Mlinga alisema kati ya miradi 137 iliyokaguliwa, ni miradi 63 tu ndiyo ilitekelezwa kwa thamani ya fedha na kwa mujibu wa mkataba.

Alisema asilimia 49 ya miradi hiyo, utekelezaji wake ulikuwa wa wastani ambapo miradi saba sawa na asilimia 5, utekelezaji wake haukuridhisha kabisa.

Sh bilioni 2 zayeyuka.



Kuhusu malipo yanayotia shaka, Mlinga alisema ukaguzi huo umebaini kuwa kuna taasisi kumi zilizofanya malipo yenye shaka ya Sh bilioni 2.1 kwa makandarasi.

Alitaja taasisi hizo kuwa ni Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga, Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero, Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya na Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro.

Nyingine ni Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga, Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Wakala wa Vizazi na Vifo (RITA), Mfuko wa Akiba kwa Wafanyakazi wa Serikalini (GEPF) na Halmashauri ya Wilaya ya Chato.

SUMA JKT yafungiwa.

Mlinga alisema PPRA pia imefungia kampuni nne kushiriki zabuni zinazotangazwa na taasisi za umma kwa mwaka mzima baada ya kushindwa kutekeleza masharti ya mikataba yao katika zabuni walizowahi kupewa na kusababisha mikataba yao kuvunjwa.

Kampuni hizo ni pamoja na Shirika la Uzalishaji JKT (SUMA JKT) ya Dar es Salaam, Vector International ya Mwanza, Shy Builders Limited ya Shinyanga na Earthline Construction Limited ya Bukoba.

TATIZO LA UPATIKANAJI WA MAFUTA LITAISHA

SERIKALI imesema hali ya upatikanaji wa mafuta imeanza kurejea katika hali ya kawaida nchini na kwamba itatoa taarifa rasmi wakati wowote kabla ya kuahirishwa kwa Mkutano wa Tisa wa Bunge la Kumi Ijumaa wiki hii.



Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliyasema hayo bungeni jana baada ya kuombwa na Spika wa Bunge, Anne Makinda ambaye alikumbushwa na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema) juu ya ahadi ya Serikali ya kulizungumzia suala la uhaba wa mafuta nchini kama ilivyokuwa imeahidi Ijumaa iliyopita, kwamba taarifa rasmi ingetolewa jana, Jumatatu.



Mnyika, baada ya kipindi cha maswali na majibu bungeni alisimama na kutumia Kanuni ya Bunge namba 68 (7) kuomba mwongozo wa Spika juu ya ahadi ya Serikali kwa kuwa suala la mafuta halikuonekana katika orodha ya shughuli za Bunge kwa siku ya jana, kama Spika alivyokuwa amemwagiza Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo wa kumtaka atoe taarifa ya Serikali ifikapo Jumatatu (jana).

Akiomba mwongozo, Mnyika alisema kuwa hali ya mafuta bado sio nzuri kwani mikoani mafuta bado hayapo na kwamba suala hili halimo hata katika orodha ya shughuli za Bunge za jana.

Mnyika alisema mbali ya taarifa ya serikali kutokuwamo katika orodha ya shughuli za bunge, lakini pia kumekuwapo na kauli zinazokinzana zinazotolewa na Waziri Muhongo na Naibu waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene.

Baada ya kutoa kauli hiyo, Spika Makinda alimtaka Waziri Mkuu kutoa taarifa kwa kuwa Waziri na Naibu wake, wote hawakuwepo bungeni.



Ndipo Waziri Mkuu alisimama na kusema kauli ya Serikali itatolewa kabla ya kuahirishwa kwa shughuli za Bunge, akisema bado inashughulikiwa, huku akiongeza kuwa, hali ya upatikanaji wa mafuta imeanza kuwa nzuri.

Hata hivyo alisema hilo haliwezi kuonekana haraka kwa watu wa mikoa ya nje ya Dar es Salaam kwa kuwa kazi ya kuyasafirisha kwa malori inachukua muda.

Petroli kufichwa Pamoja na kauli hiyo ya serikali zipo taarifa zinazodai kuwa kuadimika kwa mafuta kunatokana na vitendo vinavyofanywa na wauzaji wake za kuficha kusubiri bei mpya itakayotangazwa kesho.

Mkurugenzi wa Mpango Unaoratibu Uagizaji wa Mafuta (PIC), Michael Mjinja alielezea kushangazwa na kuadimika kwa nishati hiyo na kwamba huenda wafanyabiashara wameficha bidhaa hiyo kusubiri bei mpya.

Kauli hiyo pia imeungwa mkono na mfanyabiashara maarufu nchini, Azim Dewji ambaye alidai kuwa kero ambayo Watanzania wanaendelea kupata, imetokana na wafanyabiashara wengi kushindwa kuuza bidhaa hiyo kutokana na bei ndogo iliyopo na hivyo kukosa faida.

Wakati mafuta yakiadimika katika vituo vya reja reja, Mjinja alisema kuwa kuna mafuta mengi na ya kutosha nchini na akashangaa inakuwaje baadhi ya vituo vya mafuta kukosa nishati hiyo.

Alitoa mfano kuwa kuna meli iliyomaliza kupakua mafuta juzi na kufanya kiasi kilichopo kwenye soko la ndani kuwa ni lita milioni 33 za dizeli na lita milioni 31 za petroli na kwamba kuna meli nyingine ambayo imeanza kupakua mafuta ya ndani jana.

“Takwimu hizi ni kwa mujibu wa kampuni zinazonunua mafuta nje walizotoa jana (juzi) nashangaa kuelezwa kuwa bado kuna upungufu wa mafuta,” alisema Mjinja na kufafanua kuwa jukumu lao ni kuagiza tu nishati hiyo, ila usambazaji wameachiwa Ewura.

Tatizo hilo limekuwa kubwa mikoani, lakini pia kwa jana katika baadhi ya vituo Dar es Salaam havikuwa na nishati hiyo, jambo ambalo linadaiwa kuwa ni wafanyabiashara kuyaficha kusubiri bei mpya kesho.



Ewura imeweka utaratibu wa kutangaza bei mpya kila Jumatano ya mwanzo ya kila mwezi, hali ambayo inafanya wafanyabiashra walio wengi kuficha bidhaa hiyo kusubiri bei mpya.

Dewji alisema ukosefu wa nishati hiyo kwenye vituo vingi vya mafuta umetokana na wafanyabiashara kuona bei ya sasa haiwalipi na hata wanapotaka kuzungumza na Ewura hawafanikiwi.

“Kero yote hii imetokana na jeuri ya Ewura, hawataki kukutana na wafanyabiashara kuzungumzia suala la bei,” alisema Dewji. Bei elekezi iliyotolewa na Ewura mwanzoni mwa Oktoba, petroli ilishuka kwa Sh 306 kwa lita na Sh 192 kwa lita moja ya dizeli.

Petroli kwa Dar es Salaam inauzwa Sh 1,994 kwa lita badala ya Sh 2, 300 ya Septemba, dizeli bei yake ilishuka hadi Sh 1,950 kutoka Sh 2,142. Bei ya mafuta ya taa ilibaki Sh 1,993.

Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Ewura, Titus Kaguo hakutaka kutoa ufafanuzi wowote juu ya suala hilo la mafuta, kwa maelezo kuwa masuala yote yanazungumzwa na Wizara ya Nishati na Madini.



“Hilo suala liko ngazi ya juu, muulizeni Maswi (Eliakim-Katibu Mkuu wa Wizara) ndiye mwenye uwezo wa kuzungumzia masuala hayo,” alisema Kaguo.  Maswi alisema atatoa kauli leo kuhusu suala hilo.

Hata hivyo, baadhi ya watu wanahoji, inakuwaje wafanyabiashara hao wasubiri bei mpya bila kujua kama inashuka au kupanda na kuhisi kuwapo watu ndani ya wizara husika kuvujisha ukokotoaji unaofanyika kabla ya kutangazwa.

Lakini wapo pia wanaosema huenda wafanyabiashara hao wanatumia muda mwingi kufuatilia bei ya soko la dunia na wanapoona mwelekeo ni kupanda bei ndipo nao kidogo kidogo wanaanza kuficha nishati hiyo.

ANAYEDAIWA KUMUUA KAMANDA BARLOW ALIAGA MAITI




POLISI  imebaini kuwa mmoja wa watuhumiwa wa mauaji ya aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow, alikwenda kuaga mwili wa Kamanda huyo katika uwanja wa Nyamagana sambamba na wananchi wengine

Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Lily Matola jana alimtaja mtuhumiwa huyo kuwa ni Abdallah Petro ‘Ndayi’ (32) mkazi wa Mjimwema mjini hapa ambaye anashikiliwa Polisi.
Kwa mujibu wa Kamanda Matola, Petro mbali na kutajwa kuhusika na mauaji hayo, pia anadaiwa kuwa na rekodi ya kufungwa miaka 30 jela katika gereza la Butimba kwa unyang’anyi wa kutumia silaha mwaka 2006.
Alitoka gerezani mwaka 2010 baada ya kukata rufaa Mahakama Kuu ya Tanzania. Petro pia imebainika pia kuwa ni mdogo wa mtuhumiwa wa kwanza katika kesi hiyo, Muganyizi Peter.

Vielelezo vyakamatwa. Kamanda Matola alisema mbali na kuwa na uhusiano huo, Petro na mtuhumiwa mwingine, Abdurahim Ismail Athuman ‘Dula’ (28) mkazi wa Mkudi Ghana, pia mjini hapa, baada ya kukamatwa kwa nyakati tofauti Mjimwema na Kilimahewa mwishoni mwa wiki, waliwapeleka polisi mahali walikoficha baadhi ya mali za marehemu.
Mali wanazodaiwa kuonesha polisi ni pamoja na redio ya mawasiliano ya Polisi na funguo za gari alilotumia kamanda Barlow siku ya tukio la mauaji yake. Kamanda Matola alisema watuhumiwa waliwapeleka polisi katika shimo la majitaka kwenye maeneo ya Nyanshana, jijini Mwanza walipokuwa wameficha vitu hivyo. Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Joseph Konyo alisema watuhumiwa baada ya kutimiza uhalifu, walitenganisha redio hiyo ya mawasiliano ili isipatikane.

 “Damu ya mtu haipotei bure, hayo yote ni pamoja na Mungu mwenyewe, kwani sisi peke yetu hatuwezi, wananchi mmetusaidia sana,” alisema Kamanda Konyo.
Baada ya kuonesha polisi vitu hivyo ambavyo sasa vimechukuliwa kama vielelezo katika kesi ya mauaji ya Barlow, Kamanda Matola alisema watuhumiwa hao walipekuliwa na kukutwa pia na kadi tatu za simu za Vodacom na Airtel, simu ya mkononi, viatu vya ngozi na begi dogo.
Pia walikutwa na kofia mbili za kijeshi aina ya bereti; moja ikiwa ya Polisi na nyingine ya kampuni ya binafsi ya ulinzi, sare za kampuni ya ulinzi, mtarimbo, bisibisi, mapanga, televisheni mbili, sub-hoofer na deki.
Alisema walipohojiwa, walidai wamekuwa wakihifadhiwa na Ryoba Matiku ‘Mama Nyangi’ katika eneo la Nyakabungo Miembeni ambako mipango yote ya uhalifu imekuwa ikisukwa. Mama huyo anashikiliwa pia kwa mahojiano.

Shukurani kwa wananchi
Kamanda Konyo alisema suala la ulinzi na usalama huanzwa na wananchi kwenye familia zao na mtaa ili kujihakikishia shughuli za kutafuta riziki halali zinafanyika kwa amani na utulivu. Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyanshana Mbugani, Maduhu Lutwenya aliwaomba wananchi kurudisha uhusiano wa kutoa taarifa pale watu wasiojulikana wanapopita kwenye mitaa yao kwani mawasiliano yangekuwapo, wahalifu hao wangekamatwa nao.
“Tuwe kitu kimoja, kwani suala la usalama si la Mwenyekiti peke yake ni la kila mmoja, kwani Kamanda aliyeuawa hakuwa na hatia na mtu,” alisema.
Kukamatwa kwa watuhumiwa hao kunafanya idadi ya waliokamatwa kuhusika na kifo cha Kamanda Barlow, kuwa wanane na tayari watano wamefikishwa mahakamani.
Kamanda Barlow aliuawa usiku kati ya saa 7 na 8 Oktoba 12, katika eneo la Kitangiri kona ya Bwiru baada ya kupigwa risasi shingoni na kutokea kwenye taya na watu wanaodaiwa kuwa ni majambazi.

Sunday, November 4, 2012

MWANAFUNZI ABAKWA , ANYONGWA



WATU wawili wamekufa katika matukio mawili tofauti, mkoani Mara, akiwemo mwanafunzi mmoja wa shule ya msingi aliyebakwa na kisha kunyongwa.

Inasadikiwa wauaji wake walimnyonga kwa kutumia gauni alilolivaa na kisha kumtupa. Hayo yalisemwa na Kamanda wa polisi mkoa wa Mara, Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa polisi, Absalom Mwakyoma, akizungumza na waandishi wa habari mjini Musoma.
Kamanda Mwakyoma alisema mwanafunzi aliyebakwa na kuuawa alikuwa anasoma darasa la sita katika shule ya msingi Makoko, iliyoko katika manispaa ya Musoma na maiti yake ilitupwa eneo la Darajani manispaa ya Musoma.

Alisema kuwa uchunguzi wa awali uliofanywa na polisi na daktari inaonesha kuwa mwanafunzi huyo alibakwa kwanza kisha akanyongwa kwa gauni lake alilokuwa amevaa. Kwa mujibu wa wazazi wa mwanafunzi huyo, alitoweka nyumbani na siku mbili baadae mwili wake uliokotwa katika nyumba ambayo haitumiki. Kamanda Mwakyoma alisema hakuna watu anayeshikiliwa kuhusiana na tukio hilo. Kamanda Mwakyoma amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo, ili watu waliofanya unyama huo waweze kuchukuliwa hatua za kisheria
Katika tukio lingine mtu aliyejulikana kwa jina la Kizwere Ndege (47), amekufa papo hapo baada ya kugongwa na basi la Kampuni ya Bunda Express lenye namba za usajili T.810 eneo la Iramba, wilayani Butiama. Kamanda Mwakyoma alisema marehemu aliyekuwa akitembea kwa miguu aligongwa na basi hilo lililokuwa likiendeshwa na Mkazi wa Mwanza Ramadhan Karimu na kwamba chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi.

UJENZI WA BARABARA WATOA AJIRA 650,000



WAZIRI wa Ujenzi, Dk John Magufuli amesema miradi mikubwa ya ujenzi wa barabara inayoendelea nchini na yenye urefu wa kilometa 11, 154, imetoa ajira kwa watu 650,000.

Aidha, Dk Magufuli amesema ujenzi huo mkubwa wa barabara, ndiyo tafsiri sahihi ya kaulimbiu maarufu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Maisha Bora kwa Kila Mtanzania.
Dk Magufuli alisema tofauti na mawazo ya baadhi ya watu, miradi hiyo mikubwa ya ujenzi wa barabara inagharimiwa kwa asilimia 60 na Serikali ya Tanzania.

Waziri Magufuli aliuambia mkutano wa hadhara uliofanyika juzi katika kijiji cha Nanja mkoani Arusha wakati wa uzinduzi wa mradi wa ukarabati mkubwa wa Barabara ya Minjigu-Arusha kuwa miradi ya ujenzi pekee yake imezaa ajira 650,000. Wananchi pengine watu hawajui, lakini nataka kuwaelezeni kuwa katika Wizara moja tu ya Ujenzi kiasi cha ajira 650, 000 zimepatikana kutokana na miradi mikubwa ya barabara inayoendelea kujengwa nchini ya kiasi cha kilomita 11,154,” alisema Dk Magufuli Kuhusu maisha bora, alisema “Watu wanakejeli kaulimbiu ya maisha bora, lakini sisi katika CCM tunaposema maisha bora hakuna maana ya Serikali kugawa fedha kwa wananchi, bali ni Serikali kuwezesha wananchi. Maisha bora ni barabara, maisha bora ni usafiri wa wananchi wa uhakika kwenye barabara za lami, maisha bora ni usafirishaji mizigo usiokuwa na matatizo. Haya ndiyo maisha bora”

Aliwaambia wananchi kuwa uwezo wa Serikali kuhudumia barabara na kujenga barabara hasa za vijijini umeongezeka kwa kiasi kikubwa katika miaka saba iliyopita

Wakati uongozi wa sasa unaingia madarakani mwaka 2005, Mfuko wa Barabara ulikuwa na kiasi cha shilingi bilioni 54, lakini mwaka huu, kiasi hicho kwenye Mfuko huo kimefikia shilingi bilioni 430. Haya ni mafanikio makubwa sana na yanaongeza uwezo wa Serikali kuhudumia na kujenga barabara,” alieleza. Wakati huo huo, Rais Jakaya Kikwete janai alizindua miradi mbalimbali ya maendeleo katika mikoa ya Arusha na Manyara, ikiwa ni sehemu ya ziara zake za kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara na Singida.

Friday, November 2, 2012

MGANGA AKAMATWA KWA KOSA LA KUSABABISHA KIFO CHA MTOTO WAKATI AKIMTOA MIMBA



POLISI mkoani Mwanza inamshikilia Mganga wa Zahanati ya Kiloleli katika Kata ya Nyamanoro wilayani Ilemela, Dk Lameck Msafiri kwa kusababisha kifo cha mtoto wa miaka 15 wakati akimtoa mimba.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Lily Matola alisema Msafiri alisababisha kifo cha mtoto huyo juzi saa 3 usiku
Kwa mujibu wa Kamanda Matola, mimba ya mtoto huyo ilikuwa ya miezi minne na kabla ya kuaga duniai, alikuwa akiishi na wazazi wake katika eneo la Kilimahewa, jijini hapa. Matola alisema Dk Msafiri anashikiliwa kwa mahojiano zaidi na upelelezi ukikamilika atafikishwa mahakamani.

Wakati huo huo, wanafunzi 30 wa Shule ya Msingi Lake B pamoja na mwalimu wao wamenusurika kufa baada ya kujeruhiwa na radi kali iliyopiga juzi saa 4 asubuhi wakati wakiwa darasani
Kamanda Matola alisema ajali hiyo ilitokea wakati wanafunzi hao wa darasa la pili wakiwa darasani pamoja na mwalimu wao
Alisema walijeruhiwa na kukimbizwa katika Hospitali ya Mkoa ya Sekou Toure kwa matibabu. Alisema mwanafunzi Felix Revocatus (8) hali yake sio nzuri na amelazwa hospitalini hapo huku wengine wakitibiwa na kuruhusiwa.

Katika tukio jingine, mvua kubwa inayoendelea kunyesha jijini Mwanza imesababisha kifo cha mtoto wa miezi mitatu, Ashfat Abdsalama baaada ya mtoto huyo pamoja na wazazi wake kuangukiwa na ukuta wa nyumba wanayoishi wakati wakiwa ndani Akifafanua Kamanda Matola, alisema juzi saa 4 asubuhi katika eneo la Kirumba Mlimani B, Abdsalama Hussein (30) na mkewe Nardia Geresheni (25) pamoja na mtoto wao, walidondokewa na ukuta wa nyumba baada ya ukuta huo kudondokewa na jiwe Alisema majeruhi hao walipelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa matibabu, lakini baadaye mtoto huyo alifariki dunia na hali za baba na mama pia sio nzuri.